Habari
Wizara ya Maji Yazindua Mwongozo wa Usanifu wa Miradi ya Maji

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo amezindua Mwongozo wa Nne wa Usanifu, Ujenzi na Usimamizi wa Miradi ya Maji “Design Manual” utakaotoa utaratibu wa utekelezaji katika ujenzi wa miradi yote ya maji nchini kulingana na Sera ya Maji ya Taifa.
Prof. Mkumbo amesema lengo kuu ni kusaidia katika maandalizi ya usanifu wa miradi ya maji kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inasanifiwa, inajengwa na kusimamiwa kwa viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa, pamoja na gharama za utekelezaji wa miradi inakidhi thamani ya fedha.
Amesema mwongozo huo umezingatia mabadiliko ya tabia nchi, maendeleo ya sayansi na teknolojia, changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na awamu ya pili unaoendelea pamoja na Sheria ya Maji ya Mwaka 2019 kwa dhumuni la kufikia malengo ya kisekta wakati wa hafla ya utiliaji saini wa mikataba ya utendaji kazi baina ya Wizara ya Maji na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini.
Amefafanua kuwa kulikuwa na ulazima wa kufanyia maboresho mwongozo wa tatu kwa kuzingatia mabadiliko mbalimbali yanayotokea kwenye Sekta ya Maji, pamoja na kukabili changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini kwenye maeneo mbalimbali kama mfumo wa usambazaji wa majisafi, majitaka na maunganisho ya wateja.
Prof. Mkumbo ameipongeza timu ya Wizara ya Maji iliyofanya kazi hiyo kwa kutumia muda mfupi wa miezi saba kukamilisha kazi hiyo.
Pamoja na hilo, amezitaka Mamlaka za maji kuwekeza katika teknolojia ili kubaini dharura zinazojitokeza akitolea mfano wa changamoto ya upotevu wa maji yanayozalishwa na mamlaka za maji inayofikia asilimia 38 kulingana na ripoti ya EWURA ya mwaka 2018-2019 na kusisitiza teknolojia ikitumika ipasavyo inaweza kusaidia kubaini upotevu wa maji.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema wizara ipo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo utakaofuatilia makusanyo yote za mamlaka 69 za maji nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi wa mamlaka hizo.
Amesema mfumo huo utasaidia wizara kufuatilia na kusimamia kwa ukaribu utendaji wa mamlaka za maji kwa dhumuni la kuongeza ufanisi na kufikia malengo ya kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.