Historia


Huduma ya maji ilianza kutolewa tangu enzi za ukoloni katika miaka ya 1930. Ujenzi wa miradi ya maji kwenye vijiji ulianza mwishoni mwa miaka ya 1950 na ilitolewa katika majimbo yote tisa ya wakati huo. Mipango ya utoaji wa huduma ya maji iliandaliwa kukidhi mahitaji ya Serikali ya Mkoloni na huduma hiyo haikutolewa kwa maelekezo ya kisera. Mwaka 1961 Idara ya Maji na Umwagiliaji ilikuwa chini ya Wizara ya Kilimo, na kazi yake ilikuwa ni kutoa huduma ya maji vijijini kwa ajili ya binadamu na mifugo; utunzaji wa rasilimali ya maji na kuzuia mafuriko; kutekeleza miradi ya umwagiliaji na kufanya uchunguzi wa kihaidrolojia na kutayarisha mipango ya muda mrefu ya kuendeleza miradi ya maji.

Mwaka 1963 nchi yetu iligawanywa katika mikoa 17 badala ya majimbo tisa yaliyokuwepo wakati wa Uhuru na huduma ya maji ilianza kutolewa katika mikoa hiyo. Mwaka 1970, Sekta ya Maji ikapewa ya hadhi ya Wizara. Kazi zake zilikuwa ni pamoja na uendelezaji wa huduma ya maji vijijini na mijini. Huduma za maji ziliendelea kutolewa kupitia Idara za Maji za mikoa na wilaya chini ya uongozi wa Wahandisi wa Maji wa Mikoa na Wilaya.Mwaka 1971, Serikali ilitangaza mpango kabambe wa maji wa miaka 20 (1971-1991) wa kuwapatia wananchi vijijini maji katika umbali usiozidi mita 400.

Mara baada ya Uhuru na kwa miaka kadhaa baadaye (1961-1997) huduma za maji vijijini na mijini zilikuwa zinasimamiwa na Ofisi za Wahandisi wa Maji wa Mikoa chini ya Wizara iliyokuwa na dhamana ya maji. Utaratibu wa majaribio wa kuendesha huduma za maji mijini ulianza mwaka 1994 kwa kutumia Akaunti maalumu chini ya Sheria ya Fedha ya mwaka 1961. Majaribio hayo yalifanyika kwa miji ya Arusha, Moshi na Tanga, na yalionesha mafanikio.Kutokana na mafanikio hayo, mwaka 1998 zilianzishwa Mamlaka za Majisafi na Majitaka na hadi sasa kuna jumla ya Mamlaka 20 katika ngazi ya Miji Mikuu ya Mikoa na Mamlaka 109 katika ngazi ya Miji ya Wilaya na Miji Midogo pamoja na miradi ya Kitaifa 8 (Makonde, Handeni Trunk Main (HTM), Wanging’ombe, Maswa, Mugango Kiabakari, Chalinze na Kahama-Shinyanga, Masasi-Nachingwea).

Jiji la Dar es Salaam kwa nyakati tofauti limekuwa na usimamizi wa aina mbalimbali;Mwaka 1980 Jiji la Dar es Salaam lilikuwa linapata huduma za maji kwa kusimamiwa na Dar es Salaam Water Supply Cooperation Sole.Shirika lilikabiliwa na matatizo mbalimbali kama vile, ukosefu wa vifaa; nyenzo za kufanyia kazi; fedha; na uchakavu wa mitambo na mabomba.Mwaka 1981 Serikali ikaunda Mamlaka ya Taifa ya Maji Mijini (National Urban Water Authority-NUWA) kwa lengo la kutoa huduma nchi nzima.Huduma ilikabiliwana changamoto mbalimbali, na hivyo ikashindwa kutoa huduma ilivyokusudiwa chombo hicho kilitoa huduma katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Jiji tu. Wahandisi wa Maji wa Mikoa wakaendelea kutoa huduma kwenye Miji Mikuu ya Mikoa na Wilaya.

Mwaka 1997 Sheria ya NUWA ilifanyiwa marekebisho, na huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam ikawekwa chini ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA).

Chini ya Sheria ya DAWASA ya mwaka 2001, DAWASA ilipewa jukumu la kuhudumia Jiji la Dar es Salaam pamoja na miji ya Kibaha na Bagamoyo na eneo la kilomita mbili kila upande wa bomba kuu kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini. Katika kuboresha huduma ya maji Jijini Dar es Salaam, Serikali iliridhia DAWASA kuingia mkabata wa miaka 10 na kampuni ya City Water Services ili kuendesha huduma za majisafi na majitaka Jijini. DAWASA iliendelea kuwa mmiliki wa miundombinu. Mkataba huo ulisitishwa mwaka 2005 baada ya Kampuni ya City Water Services kushindwa kutoa huduma kwa viwango vilivyotarajiwa. Serikali ikaunda Shirika la Maji la Dar es Salaam (DAWASCO) chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992, ambapo lilianza kazi rasmi Juni, 2005.

Sera

Sera ya Maji ya mwaka 1991 ilikuwa na lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2000 wananchi wote wawe wamepata majisafi na salama kwa kiwango cha kikidhi mahitaji yao. Pamoja na mafanikio, sera ilikuwa na mapungufu yafuatayo: kutokushirikisha Sekta Binafsi na wananchi katika kupanga, kutekeleza na kusimamia miradi ya maji vijijini; msisitizo katika usambazaji wa maji kuliko utunzaji, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji; na kukosekana kwa mikakati mahsusi ya kutekeleza sera.

Sera ya Maji ya mwaka 2002: katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Sera ya Maji ya mwaka 1991, Serikali iliandaa sera nyingine ya mwaka 2002 iliyozingatia upungufu uliojitokeza katika sera ya mwanzo.

Mkakati

Mwaka 2006, Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Sekta ya Maji uliandaliwa na unalenga kuainisha majukumu ya wadau, ikiwa ni pamoja na halmashauri za wilaya; kuweka miundo ya kitaasisi; kufanya mabadiliko ya sheria; na kuainisha viwango vya uwekezaji.

Sheria

Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2009 imeweka mkazo katika ushirikishaji jamii kwenye utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira; na wananchi kupewa fursa ya kuunda vyombo vya watumiaji maji na kuvisajili kwa Msajili ambaye ni Mkurugenzi wa halmashauri husika.

Sheria Na.5 ya mwaka 2019 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, pamoja na mambo mengine, ilianzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambayo ilichukua majukumu yaliyokuwa hapo awali yamekabidhiwa kwa OR-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Majukumu yaliyohamishwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwenye jamii za watu waishio maeneo ya vijijini, miji midogo na Makao Makuu ya Wilaya.

Pamoja na hilo, Sheria Na.5 ya mwaka 2019 imehamisha uwajibikaji wa maafisa wanaohusika na utoaji wa huduma ya maji kutoka OR-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda Wizara ya Maji. Wakala mpya iliyoanzishwa (RUWASA) ina ofisi ngazi za Makao Makuu Dodoma, Mikoa na Wilaya. Hii ni tofauti na muundo wa hapo awali ambao ulikuwa unajumuisha ofisi katika ngazi ya Serikali za Mitaa (LGAs) na Sekretarieti za mikoa (RSs).

RUWASA ilianza kazi tarehe 1 Julai 2019

Matukio Muhimu

(i) Matumizi ya mianzi miti katika kusambaza huduma ya maji. Teknolojia hiyo ilionekana kuwa na udhaifu kwa kuhitaji dawa nyingi kuihifadhi mianzi, pamoja na waya kwa ajili ya kuzuia isipasuke;

(ii) Mikutano ya Mwaka ya Maji ilianzishwa mwaka 1980 (Annual Water Experts Conference);

(iii) Vijiji kuunda kamati za maji kwa mujibu wa Sera ya Maji ya mwaka 2002.

Bofya kusoma takwimu muhimu