Habari

Imewekwa: Mar, 10 2026

Waziri Mkuu Aitaka Wizara ya Maji Kutumia Mitambo ya Serikali Kuharakisha Miradi ya Maji

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ameitaka Wizara ya Maji kutumia kikamilifu na kwa tija mitambo ya kuchimba visima iliyonunuliwa na Serikali, ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maji na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Rukwa, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa na wa kimkakati kwa kununua mitambo 25 ya kisasa ya kuchimba visima, sambamba na mitambo ya kuchimba mabwawa na ile ya kufanya utafiti na upimaji wa vyanzo vya maji. Alibainisha kuwa uwekezaji huo unalenga kuongeza kasi, ufanisi na uhuru wa Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuendelea kukodi mitambo kutoka sekta binafsi wakati Serikali tayari imewekeza rasilimali kubwa katika kununua vifaa vyake. “Mitambo hii ni mali ya Watanzania na lazima itumike ipasavyo kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi,” alisisitiza, huku akiitaka Wizara kuweka mfumo thabiti wa usimamizi, upangaji kazi na ufuatiliaji ili kuhakikisha matumizi yake yanaendana na malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, Waziri Mkuu amekumbusha agizo lake la kuhakikisha vituo vyote vya huduma za jamii—ikiwemo shule, vituo vya afya na taasisi nyingine muhimu—vinapatiwa huduma ya majisafi na salama ndani ya kipindi cha miezi sita. Ameweka wazi kuwa hatasita kuchukua hatua kali za kiutawala dhidi ya yeyote atakayeshindwa au kupuuza utekelezaji wa agizo hilo.

Ameeleza kuwa usambazaji wa mitambo hiyo katika mikoa yote ya Tanzania ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuharakisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi, kupunguza utegemezi wa huduma za nje, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa gharama nafuu na kwa wakati.

Kwa ujumla, amesisitiza kuwa utekelezaji madhubuti wa miradi ya maji ni nguzo muhimu katika kuboresha afya za wananchi, kuchochea shughuli za kiuchumi, na kuinua ustawi wa jamii, hivyo Wizara ya Maji ina wajibu wa kuhakikisha uwekezaji huu unaleta matokeo halisi na endelevu kwa Watanzania wote.