Habari

Imewekwa: Dec, 04 2019

Wizara ya Maji Yaweka Kambi Misungwi kutatua Changamoto ya Maji

News Images

Mwanza; 03 Desemba, 2019

TAARIFA KWA UMMA

Uongozi wa Wizara ya Maji ukiongozwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga pamoja na wataalam wa Wizara ya Maji wameweka kambi katika Wilaya ya Misungwi kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa Mradi wa Maji Mbalika, mkoani Mwanza.

Hatua hiyo imekuja baada ya utekelezaji wa mradi huo kukwama kutokana na kuchelewa kufika kwa mabomba ya chuma (steel pipes) kutoka kiwandani, jambo lililomlazimu Naibu Waziri Aweso kuitisha kikao cha dharura kitakachofanyika kesho tarehe 05 Desemba, 2019 kitakachohusisha Kiwanda cha Tanzania Steel Pipe (TSP), wasimamizi wa mradi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na mkandarasi; Kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corporation ya China kwa dhumuni la kupata muafaka mradi ukamilike.

Aweso amesema hataondoka katika Wilaya ya Misungwi mpaka atakapo hakikisha fedha za ununuzi wa mabomba hayo zimelipwa ili kazi ya ulazaji wa mabomba na kazi zote zilizobaki, sawa na asilimia 29 ziishe. Na akatoa agizo kuwa mradi uwe umekamilika ifikapo mwezi Machi, 2020 tayari kuhudumia watu zaidi ya 81,800 katika vijiji vya Nyang’homango, Isesa, Igenge na Mbalika.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Aweso ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Misungwi uliokuwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), ambao ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99 na kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 12.

Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga ameishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha kwa wakati, pamoja na usimamizi mzuri jambo lililosababisha mradi huo kukamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachoakisi thamani halisi ya fedha zilizotumika.

Akisema mradi huo utamaliza kero ya maji ya mji wa Misungwi na kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi 64,000 waishio katika mji mdogo wa Misungwi, vijiji vya Nyahiti, Mapilinga na Mwambola mpaka kufikia mwaka 2032.

Kitengo cha Mawasiliano