Habari
Wataalamu wa RUWASA Wajengewa Uwezo Kuhusu Uendeshaji na Matengenezo ya Skimu za Maji
Wahandisi na wataalamu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wanapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua katika miundombinu ya usambazaji wa maji.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa RUWASA, Mhandisi Aziz Mutabuzi, amesema mafunzo hayo yanahusu uendeshaji na matengenezo ya skimu za maji vijijini ili kuhakikisha miradi ya maji inafanya kazi kwa ufanisi na kwa muda mrefu.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanafanyika kwa ushirikiano kati ya RUWASA na shirika la Global Water Center, ambalo linatoa utaalamu kuhusu matumizi ya nishati ya jua katika miradi ya maji.
Kwa upande wake, Mhandisi Kogi Chege kutoka Global Water Center amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi kwa wahandisi pamoja na waratibu wa matengenezo ya miundombinu ya maji, ili waweze kusimamia kwa ufanisi mifumo ya maji inayotumia nishati ya jua.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanahusisha wahandisi kutoka mikoa 25 inayosimamiwa na RUWASA katika utoaji wa huduma za maji vijijini, ambapo hadi sasa washiriki kutoka mikoa 16 tayari wamepatiwa mafunzo.
Aidha, mafunzo hayo pia yanajumuisha mbinu za kutibu maji ili kuhakikisha maji yanayowafikia wananchi ni salama kwa matumizi.
Wahandisi waliopata mafunzo wanatarajiwa kupeleka elimu hiyo katika ngazi za wilaya na vijiji ili kusaidia jamii kupata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.

