Habari

Imewekwa: Sep, 01 2022

Wizara ya Maji Kutekeleza Mradi wa Bilioni 134 katika Miji ya Tarime na Rorya

News Images

Wizara ya Maji imeingia mkataba wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 134 na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji katika miji ya Rorya na Tarime, mkoani Mara.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini ya utekelezaji wa mradi huo Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kazi hiyo inatarajiwa kuchukua miezi 30, lakini akamtaka mkandarasi atumie muda mfupi zaidi kukamilisha kazi hiyo.

Waziri Aweso amesema mradi huo ni muendelezo wa utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kumaliza kero ya maji kwa wananchi wa mkoa Mara na kuuomba uongozi na wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano ili mradi huo uweze kukamilika haraka.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema mradi huo utahusisha kazi za ujenzi wa chanzo cha maji, chujio la kutibu maji, ulazaji wa mabomba makubwa ya kusafirisha na kusambaza maji, ujenzi wa matenki, vituo vya kusukuma na kuchotea maji.

Mhandisi Sanga amesema ujenzi wa mradi huo itachukua muda wa miezi 30 na utanufaisha wananchi 460,885 katika halmashauri za Rorya na Tarime.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation, Zhang Junle amesema kuwa wana uzoefu wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji nchini kama Magu, Lamadi na Ngudu.

Akiishukuru Serikali kuiamini kwa kuwapa kazi hiyo, akisisitiza kuwa watafanya kazi hiyo kwa wakati na viwango.