Habari

Imewekwa: Jun, 08 2026

Wizara ya Maji Yatakiwa Kutekeleza Miradi kwa Kuzingatia Uhifadhi wa Ardhi Oevu

News Images

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Emmanuel Nchimbi, ameielekeza Wizara ya Maji kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi ya maji nchini unazingatia uhifadhi na ulinzi wa ardhi oevu.

Agizo hilo alilitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, ambapo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais alisema kuwa Tanzania inatarajiwa kuwa na zaidi ya watu milioni 100 ifikapo mwaka 2050. Alisisitiza kuwa uhifadhi wa ardhi oevu ni muhimu katika kulinda na kuendeleza vyanzo vya maji, pamoja na kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa maji nchini.

Aidha, aliiagiza Tanzania Forest Services Agency (TFS) kuhakikisha upandaji wa miti unaimarishwa katika maeneo mbalimbali ili kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji. Alibainisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka kipaumbele katika masuala ya mazingira na uhifadhi wa ardhi oevu.

Katika maagizo mengine, Makamu wa Rais alizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuanzisha na kutunza bustani za kijani kama sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira na kuongeza ustawi wa jamii.

Maadhimisho hayo pia yalihusisha uzinduzi wa Programu Endelevu ya Usimamizi wa Mazingira kuelekea Dira ya Taifa 2050, ambayo itatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030 kwa lengo la kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini.