Habari
Waziri wa Maji Aivunja Menejimenti ya MWAUWASA
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), ameivunja Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kufuatia kutoridhishwa kwake na kiwango cha utoaji huduma ya majisafi na salama jijini Mwanza.
Uamuzi huo umefuatia ziara ya kikazi aliyoifanya jijini Mwanza, ambapo amebaini uwepo wa changamoto za upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi, changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na udhaifu wa kiutendaji.
Akizungumza na watumishi wa MWAUWASA, Waziri Aweso amesema kuwa licha ya mamlaka hiyo kuwa miongoni mwa taasisi bora za maji nchini, utendaji wake wa sasa hauendani na matarajio ya Serikali na wananchi.
“Kwa sasa siridhishwi na utendaji wa MWAUWASA na nyinyi wenyewe mmekiri. Asilimia kubwa ya changamoto nilizobaini kwenye ziara yangu ni za kiutendaji,” Aweso amesema.
Ameongeza kuwa amekuwa akitoa maelekezo mara kwa mara kwa menejimenti ya MWAUWASA kuhusu umuhimu wa uwajibikaji na kuongeza ufanisi, lakini hakuna mabadiliko aliyoyaona.
“Naivunja menejimenti ya MWAUWASA na kuanza upya. Tutatengeneza timu mpya ya watendaji kwa dhumuni la kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi wa taasisi hii muhimu,” Aweso amesisitiza.
Waziri Aweso amefafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha menejimenti mpya itakayoundwa itawajibika kikamilifu katika kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Mwanza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema Wizara haitasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi wasiowajibika katika maeneo yote nchini.
“Wizara itaendelea kufuatilia utendaji kwa karibu. Nawasisitiza watumishi wa MWAUWASA kubadilika, kwani uwajibikaji wenu ndio utakaopunguza changamoto zinazowakabili wananchi,” amesema Mhandisi Mwajuma.

