Habari
Teknolojia ya Kurejesha Majitaka kwa Matumizi Mengine Yajadiliwa na Wadau wa Sekta ya Maji
Wadau wa Sekta ya Maji wamejadili teknolojia na mbinu mbalimbali za kutibu na kurejesha majitaka kwa matumizi mengine yenye manufaa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji nchini.
Majadiliano hayo yalifanyika katika kikao jumuishi kilichoandaliwa na Wizara ya Maji jijini Dodoma, kikilenga kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho bunifu la kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji kutokana na ongezeko la mahitaji.
Wadau hao walieleza kuwa kiasi kikubwa cha maji hupotea kama majitaka yanayotokana na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo viwanda, makazi ya watu na taasisi za elimu. Walisema kuwa kwa kutumia teknolojia sahihi, maji hayo yanaweza kutibiwa na kutumika tena kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha, walisisitiza kuwa kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji, kuna umuhimu wa kuendelea kubuni na kuwekeza katika teknolojia za kisasa zitakazowezesha matumizi bora ya majitaka yaliyotibiwa na kuyageuza kuwa rasilimali muhimu kwa matumizi ya sasa na ya baadaye.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Bw. Robert Sunday, alisema kuwa matumizi ya majitaka yaliyotibiwa yanaweza kuleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali na kusaidia kupunguza shinikizo la matumizi ya vyanzo vya maji asilia.
Bw. Sunday aliongeza kuwa usimamizi bora wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji unapaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama kwa maendeleo endelevu ya taifa.

