Habari

Imewekwa: Apr, 27 2023

Waziri wa Maji ataka Watumishi wapewe nafasi

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema ni muhimu kwa viongozi wa Sekta ya Maji kuwapa nafasi watumishi na kuongea nao ili waonyeshe ujuzi wao katika kazi.

Amesema hayo wakati wa kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Maji jijini Dodoma ambapo amesisitiza kiongozi anatakiwa awe faraja kwa watumishi na asitumie nafasi kutisha watumishi.

Amesema watumishi hawatakiwi kuwaogopa viongozi katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kazi na yale ya kijamii.

Waziri Aweso amesema ni muhimu viongozi kutathmini watendaji katika maeneo ya kazi na kushikama katika utekelezaji wa kazi ili kuimarisha Sekta ya Maji

Waziri Aweso amesema Sekta ya Maji bado ina kazi kubwa ya kufanya kwasababu uchumi wa nchi unakua na mahitaji yanaongezeka.

Amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi katika mafunzo mbalimbali, ikiwamo mabadiliko ya tabia nchi ili kutoa majibu Kwa changamoto mbalimbali katika Sekta ya Maji.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiongea awali amesema Wizara ya Maji imejikita katika matumizi vyanzo vya maji vya uhakika kama vile maziwa na mito mikubwa.

Amesema lengo no kufikisha huduma ya maji ya uhakika Kwa wananchi kama Serikali ilivyopanga.

Kuhusu hilo, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema pamoja na utekelezaji wa kazi kwa weledi na kiwango, maslahi ya Watumishi wa Sekta ya Maji yatafanyiwa kazi kwa uhakika na wakati.

Kitengo cha Mawasiliano