Habari

Imewekwa: May, 27 2021

Waziri Aweso Asikiliza Changamoto za Wadau wa Uchimbaji Visima

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amekutana na wadau na wakandarasi wa uchimbaji visima kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Waziri Aweso amekutana na wadau hao katika kikao cha siku moja kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho pia kimetumika kuongeza uelewa kwa wadau kuhusu namna bora ya kusimamia rasilimali za maji.

Waziri Aweso baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wachimbaji wa visima na watafiti wazawa ameona kuna haja ya kuwakutanisha na Wizara ambazo zinashirikiana hususan katika sekta ya maji kwa ajili ya kukaa pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

“Kuwe na utaratibu wa kukutana ili kama kuna changamoto tuweze kuzitatua na kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya maji,” Waziri Aweso amesema.

Amesema wakati umefika sasa wa kuhakikisha Makampuni yote yanayofanya kazi za uchimbaji visima yanasajiliwa ili Wizara iweze kuwatumia katika shughuli za uchimbaji visima hasa katika maeneo ya vijijini ili wananchi waweze kupata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Aidha, Waziri Aweso amesema umefika wakati sasa Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA) kuainisha uwezo wake wa idadi ya visima wanavyoweza kuchimba kwa mwaka ili visima vinavyobaki wakabidhiwe wachimbaji wazawa ambao kwa pamoja wataongeza kasi ya utekelezaji wa kuchimba visima kwa haraka na kuweza kuwapatia wananchi majisafi na salama.

Amesisitiza kwamba (DDCA) ifanye utaratibu wa kuwatambua wachimbaji binafsi ambao watawatumia katika kusaidia kazi ya uchimbaji visima ili kurahisisha kazi ya kuwapatia wananchi huduma ya majisafi.

Waziri Aweso amebainisha kuwa eneo lingine ambalo wakandarasi wanataka kusikia ni kuhusu suala zima la malipo yao, wanataka wanapofanya kazi walipwe kwa wakati, isijengeke tabia kufanya kazi na kulipwa ni hisani.

Katika hilo, Waziri amewaagiza wadau hao kuwa yeyote ambaye ana madai yake ambayo hajalipwa kabla hajaondoka Dodoma awasilishe hati za madai hayo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, pia kuhakikisha Wizara inafungua ukurasa mpya katika kutekeleza miradi ya maji nchini pamoja na wadau hao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Rasimali za Maji, Dkt. George Lugomela amesema kikao hicho kimelenga kuwaleta pamoja wamiliki wa makampuni 60 ambayo yamesajiliwa na Wizara ili kuleta uelewa wa pamoja katika suala zima la utafiti na maji chini ya ardhi.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema watafiti na wachimba visima ni wadau wa Wizara ya Maji na kwamba Wizara inawategemea katika kufanya kazi nao kwa pamoja ili kuleta mafanikio na mageuzi katika sekta ya maji nchini.

Kitengo cha Mawasiliano