Habari

Imewekwa: Jan, 31 2026

Waziri Aweso Asisitiza Ufanisi na Tija kwa Bodi za Maji za Mabonde

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amezisistiza Bodi za Maji za Mabonde nchini kuimarisha ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha ufanisi na matokeo yenye tija katika usimamizi wa rasilimali za maji.

Akizungumza katika kikao kazi na viongozi wa Bodi za Maji za Mabonde kilichofanyika jijini Dodoma, Waziri Aweso amewataka Wakurugenzi na watumishi wa bodi hizo kuzingatia malengo makuu ya Wizara ya Maji na kutekeleza majukumu yao kwa kuongozwa na viashiria vya utendaji kazi (KPI’s) vinavyoleta matokeo chanya kwa Taifa.

“Nasisitiza utekelezaji wa majukumu yenu unapaswa kuendana na malengo makuu ya Wizara ya Maji, ikiwemo kufanikisha mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji, ili kuimarisha usalama wa maji nchini,” Waziri Aweso amesema.

“Bodi za Maji za Mabonde zinapaswa kushirikishwa kikamilifu katika kutekeleza malengo ya sekta, zikitumia rasilimali za maji kama nyenzo ya kuchochea uchumi wa Taifa”, Aweso amesisitiza.

Kuhakikisha uwajibikaji kwa umma, Waziri Aweso amesisitiza kuwa kazi zinazotekelezwa na mabonde zinapaswa kuwa wazi, zikitoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya bodi, umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji na matumizi endelevu ya rasilimali hizi.

Vilevile, amewataka viongozi wa bodi hizo kuzingatia uadilifu, heshima ya taasisi, nidhamu ya kazi, na kuishi karibu na wananchi ili kulinda imani ya umma. Pia amesisitiza udhibiti wa uchimbaji holela wa visima na ujenzi wa mabwawa kwa kushirikiana na wadau na wananchi, kwa lengo la kulinda rasilimali za maji na mazingira kwa ujumla.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesisitiza kuimarishwa kwa mahusiano ya kisekta, nidhamu kazini, na ushirikiano wa utendaji kazi miongoni mwa watendaji wa Sekta ya Maji.

Amehimiza pia ushirikiano wa karibu kati ya Bodi za Maji za Mabonde na Idara ya Ubora wa Maji katika kutoa huduma bora kwa jamii.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amemteua Bi. Bona Mremi kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Bonde la Ziwa Tanganyika, ambaye awali alikuwa Meneja Mazingira na Uratibu wa Jumuiya za Watumia Maji katika Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika.