Habari
Waziri Aweso Aanika Mafanikio ya Sekta ya Maji
Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb), amesema kuwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yameendelea kuwa dira kuu ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya Awamu ya Sita, hususan katika Sekta ya Maji ambayo ni mhimili muhimu wa afya ya jamii, uzalishaji, ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa.
Waziri Aweso ameyasema hayo wakati akichangia mjadala wa Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyotolewa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu tarehe 14 Novemba 2025.
Akichangia mjadala huo, Waziri Aweso amesema Serikali imeongeza uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Maji, hatua iliyowezesha upatikanaji wa maji safi na salama kufikia zaidi ya asilimia 91 kwa maeneo ya mijini na takribani asilimia 83 kwa maeneo ya vijijini, ikilinganishwa na viwango vilivyokuwepo kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Katika mchango wake, Waziri Aweso ameainisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maji inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo:
- Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria – Mwanza, unaohudumia Jiji la Mwanza na maeneo ya jirani, ukiwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya maji nchini.
- Mradi wa Maji wa Same–Mwanga–Korogwe, unaolenga kuondoa kabisa changamoto ya maji katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.
- Mradi wa Maji wa Makonde Plateau, unaohudumia Mikoa ya Mtwara na Lindi, ukiwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji katika ukanda wa kusini.
- Mradi wa Maji wa Chalinze, unaohudumia Chalinze, Bagamoyo, Handeni na maeneo ya jirani, ukiimarisha upatikanaji wa maji katika ukanda wa Pwani.
- Mradi wa Maji wa Mtwara–Mikindani, unaolenga kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Mtwara na maeneo ya jirani.
- Mradi wa Maji wa Tabora–Nzega–Igunga, unaohudumia Mkoa wa Tabora na kusaidia kupunguza tatizo la maji katika ukanda wa kati.
- Mradi wa Maji wa Farkwa–Dodoma, unaotarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma na maeneo yanayokua kwa kasi ya makazi na shughuli za kiuchumi.
Akizungumza kuhusu miradi mingine, Waziri Aweso amesema, “Pamoja na miradi hii mikubwa, Serikali inaendelea kutekeleza maelfu ya miradi ya maji ya kati na midogo katika vijiji, miji na majiji mbalimbali nchini, hatua iliyosaidia kuwapunguzia wananchi umbali na muda wa kufuata maji.”
Katika usimamizi wa rasilimali za maji, Waziri Aweso amesema Serikali imeimarisha ulinzi wa vyanzo vya maji kupitia Bodi za Maji za Mabonde, jambo lililosaidia kupunguza migogoro ya matumizi ya maji, kulinda mazingira na kuhakikisha uendelevu wa rasilimali hiyo muhimu.
Ameongeza kuwa, “Serikali imeendelea kuimarisha taasisi zote katika Sekta ya Maji kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya mita za maji za malipo ya kabla na mifumo ya kielektroniki ya usimamizi, hatua iliyoongeza ufanisi, uwazi na ukusanyaji wa mapato.”
Akihitimisha mchango wake, Waziri Aweso amesema Wizara ya Maji itaendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo yote ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na mipango ya kitaifa vinaendelea kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa Sekta ya Maji.
Waziri Aweso ametoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda, kutunza na kusimamia vyanzo na miradi ya maji, akisisitiza kuwa maji ni haki ya msingi ya kila Mtanzania na msingi wa maendeleo endelevu ya Taifa.

