Habari
Mhandisi Mwajuma Awataka Bodi ya Taifa ya Maji Kutembelea Miradi ya Maji
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ameitaka Bodi ya Taifa ya Maji kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu Sekta ya Maji.
Akizungumza katika kikao cha kwanza cha Bodi ya Tano (5) ya Taifa ya Maji, kilichofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba jijini Dodoma, Mhandisi Mwajuma alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya bodi hiyo na Wizara katika uandaaji na utekelezaji wa miradi ya maji.
Mhandisi Mwajuma amesema kuwa wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Maji wamebeba dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Alisisitiza kuwa mafanikio katika sekta ya maji yanapatikana kupitia ushirikiano wa karibu na mipango ya pamoja.
“Maji ndio kichocheo cha ukuaji wa nchi kama inavyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya 2050. Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ni muhimu kwa kuboresha maisha ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha malengo haya yanafikiwa,” Mhandisi Mwajuma amesema.
Aidha, aliwahimiza wajumbe wa bodi kuwa mabalozi wazuri katika shughuli mbalimbali za sekta, ikiwemo utunzaji, uhifadhi, mgawanyo na usimamizi wa rasilimali za maji.
Mhandisi Mwajuma ameongeza kuwa upungufu wa maji huathiri jamii, mifugo na kilimo, hivyo ni muhimu kuwa na mipango mkakati ya kukabiliana na changamoto zinazotokea katika vyanzo vya maji.
Amewapongeza wajumbe wa bodi hiyo kwa uteuzi wao na kuwaahidi kwamba ushauri wao utazingatiwa ili kuleta maendeleo katika Sekta ya Maji.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Maji, Hussein Ally, alisema bodi hiyo itatoa ushirikiano na maoni katika masuala mbalimbali, ikiwemo utafutaji wa vyanzo mbadala vya fedha za ujenzi wa miradi ya maji na uthibiti wa upotevu wa maji.
Amesisitiza utendaji wa bodi hiyo kuzingatia weledi na weledi wa kazi ili kuhakikisha Sekta ya Maji inakuwa moja ya sekta muhimu katika maendeleo ya Taifa.

