Habari

Imewekwa: Sep, 06 2021

Waziri Aweso Afanya Mazungumzo na Balozi wa India

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa miji 28 wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 500 unaotarajiwa kuanza karibuni katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Maji, Mtumba, jijini Dodoma.

Mhe. Aweso amemuomba Balozi Pradhan kuwezesha utekelezaji mzuri wa mradi mkubwa na muhimu wa kihistoria utakaoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Maji Tanzania, unaotarajiwa kuanza punde uweze kukamilika haraka iwezekanavyo na ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa.

Vilevile, ameishukuru Serikali ya India kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi wa maji wa Igunga, Nzega na Tabora kwa kutoa fedha za mkopo wa masharti nafuu kupitia Exim Bank ya India pamoja na wakandarasi kutoka India waliofanya kazi nzuri na kuwezesha mradi kukamilika kwa wakati na kiwango bora.

Pia, ameiomba India kuendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania kwenye Sekta ya Maji katika maeneo mbalimbali kwa dhumuni la kuinua kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama nchini.

Aidha, Balozi Binaya Srikanta Pradhan amemuhakikishia Waziri Aweso ushirikiano mkubwa kutoka Serikali ya India kwenye maeneo mbalimbali ya kisekta pamoja na kuwajengea uwezo wataalam kwenye maeneo kukabiliana na upotevu wa maji, usimamizi na uendeshaji wa miradi na ujenzi wa miradi.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga pamoja na viongozi wa idara wizarani hapo.