Habari

Imewekwa: Feb, 02 2026

Sekta ya Maji Yaazimia Kufanya Mageuzi Makubwa ya Kidigitali

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema Sekta ya Maji imejipanga kufanya mageuzi makubwa ya kidigitali kwa kuwekeza katika mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

Amesema kipaumbele cha Wizara ya Maji kwa sasa ni kuboresha huduma kwa wateja, hivyo itaendelea kuimarisha mifumo yake ya mawasiliano ili kutatua changamoto mbalimbali za sekta hiyo kwa njia ya kidigitali.

Waziri Aweso ameyasema hayo wakati wa kikao kati yake na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, pamoja na Menejimenti za Wizara ya Maji na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuimarisha mifumo ya kiteknolojia katika Sekta ya Maji ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, na kilifanyika Makao Makuu ya Wizara ya Maji jijini Dodoma.

“Ni lazima tuwekeze katika mifumo ya teknolojia ya habari ili kukabiliana na changamoto za upotevu wa maji, maunganisho ya wateja, ankara zisizo halali, wizi wa maji pamoja na upotevu wa mapato katika taasisi zetu,” Aweso amesisitiza.

Aidha, ameeleza kuwa Wizara inalenga kuboresha mifumo ya mawasiliano katika Sekta ya Maji ili mifumo yote ya kisekta na taasisi zake iweze kuwasiliana na kusomana kwa ufanisi, pamoja na kuunganishwa na mifumo mingine nje ya sekta kwa lengo la kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa utendaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Anjela Kairuki, amesema Sekta ya Maji ni miongoni mwa sekta muhimu na za kipaumbele, hivyo ni lazima kuwa na Mfumo bora wa Mawasiliano wa Maji wa Kidijitali.

Ameeleza kuwa mfumo huo utawezesha kupunguza upotevu wa maji, kuongeza ufanisi katika makusanyo ya ankara za maji, matumizi sahihi ya maji, pamoja na kupunguza wizi wa maji na uvujaji.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema Kitengo cha TEHAMA cha Wizara ya Maji kimefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa mifumo mbalimbali na kuahidi kukiimarisha zaidi ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Amesisitiza kuwa mifumo bora ya mawasiliano ni muhimu kwa taasisi, kwani upatikanaji wa taarifa sahihi husaidia kufanya maamuzi sahihi na kuimarisha utendaji wa kila siku wa taasisi.