Habari

Imewekwa: Apr, 18 2025

Mkandarasi Bwawa la Itaswi-Kisaki Kondoa Kulipwa Madai Yake

News Images


Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemuagiza Mtendaji Mkuu Mfuko wa Maji wa Taifa, Haji Nandule kumlipa mkandarasi Canopies International (T) LTD anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Bwawa la Itaswi-Kisaki wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma shilingi milioni 700 ili mradi huo ukamilike kwa haraka.

Agizo hilo amelitoa baada ya kupokea malalamiko ya kuchelewa kwa mradi kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Amesema ucheleweshaji wa malipo ya mkandarasi wakati ambapo fedha zipo hauvumiliki na hivyo watendaji wa wizara wahakikishe changamoto kama hizo zinapatiwa ufumbuzi wa haraka. Amesisitiza kuwa lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanatuliwa ndoo kichwani liko paleplae hivyo watendaji wasikwamishe.

Waziri Aweso amesema bwawa hilo lina umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kondoa kwa sababu kukamilika kwake litaondoa changamoto ya huduma ya maji katika kata 6 zenye vijiji 20 na litawezesha upatikanaji wa maji kwa asilimia mia moja kwa kipindi chote cha mwaka.

Bwawa hilo linatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.7 limefikia asilimia 33 huku likitarajiwa kukamilika Oktoba 2025.

Naye Mbunge wa Kondoa Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi wilayani hapo. Amesema ndani ya miaka Minne serikali imeleta zaidi ya bilioni 19 kwa ajili ya miradi mbalimbali jambo ambao limeifanya wilaya ya Kondoa kupiga hatua kubwa katika maendeleo