Habari

Imewekwa: Apr, 29 2025

RUWASA Iringa Yang’ara na Mradi wa Maji Itagutwa

News Images

Mwenge wa Uhuru umekagua na kuzindua rasmi Mradi wa Maji wa Itagutwa, uliotekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Iringa. Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya majisafi, salama na ya uhakika.

Mradi wa Itagutwa ni upanuzi wa skimu ya awali iliyokuwa ikihudumia Kijiji cha Kinywang’ang’a kwa kutumia chanzo cha maji kutoka Kijiji cha Itagutwa. Kupitia upanuzi huu, uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka hadi kufikia lita 10,440 kwa saa, sawa na lita 250,560 kwa siku. Hii ni zaidi ya mara mbili ya mahitaji ya sasa ya maji kwa siku katika eneo hilo, ambayo ni lita 108,030, hivyo kuweka msingi imara wa huduma endelevu kwa jamii hiyo.

Mradi huo umegharimu Shilingi milioni 322.07 na kufadhiliwa kupitia fedha za Programu ya Malipo kwa Matokeo (PforR), chini ya usimamizi wa Wizara ya Maji. Kwa sasa, mradi unahudumia moja kwa moja wakazi 1,645 wa Kijiji cha Itagutwa, ambao hapo awali walikumbwa na changamoto ya kutumia muda mwingi kutafuta maji, hali iliyokuwa ikipunguza ufanisi katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Utekelezaji wa mradi ulianza rasmi mwezi Mei 2023 na ulikamilika ndani ya miezi sita kama ilivyopangwa. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 75,000, uchimbaji wa mitaro, ulazaji na ufukiaji wa bomba lenye urefu wa kilomita 12.75, ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji pamoja na ukarabati wa banio la maji (intake).

Skimu hii sasa inaendeshwa na Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) kiitwacho Kiwele, ambacho kimepewa jukumu la kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kutolewa kwa ufanisi na kwa viwango vinavyokubalika.

Kupitia mradi huu, RUWASA Iringa imeonesha mfano bora wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye kugusa maisha ya wananchi kwa karibu. Zaidi ya kuboresha hali ya upatikanaji wa maji, mradi huu umeongeza matumaini na kuleta heshima kwa wakazi wa Itagutwa, ambao sasa wanaweza kutumia muda wao kufanya shughuli nyingine za kujiletea maendeleo.