Habari
Ushirikiano wa Tanzania na Qatar Kuimarisha Huduma ya Majitaka Nchini

Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Dodoma (DUWASA), Mtwara (MTUWASA) na Ubalozi wa Tanzania Nchini Qatar zimeahidiwa ushirikiano katika eneo la Usafi wa Mazingira hususani suala la udhibiti na uondoshaji wa majitaka.
Katika mazungumzo na ujumbe kutoka Tanzania ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA), Mhandisi Rejea Ng’ondya ameishukuru nchi ya Qatar kwa kuonesha nia katika usimamizi wa mifumo ya usafi wa mazingira katika mamlaka za maji.
Mkurugenzi wa Mifumo ya Majitaka wa Taasisi ya (ASHGAL) kutoka Qatar, Abdulaziz Ahmad, ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Qatar zimekuwa na ushirikiano mazuri ya muda mrefu katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kiuchumi kwa manufaa ya nchi zao.
“Tunatambua misingi imara ya muda mrefu iliyowekwa na watangulizi wetu katika kuimarisha mahusiano. Sisi kama Taasisi ya mifumo ya Majitaka tunaahidi kusaidiana na Tanzania katika upande wa wataalam wa technolojia ya mifumo” Ahmad amesisitiza
Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Habibu Awesi Mohammed, amezishukuru Mamlaka za Maji za DAWASA, DUWASA na MTUWASA na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambao nao wameshiriki katika ziara hiyo kwa kuonesha nia ya kujifunza nchini Qatar juu ya usimamizi wa mifumo ya usafi kwa manufaa ya watanzania.