Habari

Imewekwa: Apr, 29 2025

Mafunzo Elekezi kwa Waajiriwa Wapya ni Muhimu katika Kuimarisha Utumishi wa Umma

News Images

Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma imeratibu mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa wizara hiyo. Mafunzo hayo yamehusisha watumishi wapya 60 na kufanyika katika Mji wa Serikali jijini Dodoma.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanatoa elimu muhimu kuhusu misingi ya utumishi wa umma, sheria, kanuni, taratibu, na maadili yanayopaswa kuzingatiwa na kila mtumishi wa umma. Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu, Bi. Christina Akyoo, alisema kuwa mafunzo haya ni utekelezaji wa takwa la kisheria kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma.

Bi. Akyoo alieleza kuwa mafunzo haya yatasaidia waajiriwa wapya kuelewa wajibu wao katika kutoa huduma bora kwa wananchi, kujiepusha na vitendo vya rushwa, kutunza siri za serikali, pamoja na kuimarisha utendaji kazi wa pamoja uliojaa upendo, mshikamano na maadili ya kitaaluma.

Aidha, alisisitiza kuwa kupitia mafunzo haya, watumishi wapya watakuwa sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.

Miongoni mwa kada zilizoshiriki katika mafunzo haya ni pamoja na waandishi wa habari, waendesha ofisi, wahandisi, madereva na wataalamu wa ubora wa maji.