Habari

Imewekwa: Dec, 08 2021

Wataalam wa Rasilimali za Maji Watakiwa Kuelewa Mabadiliko ya Tabiachi

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewataka wataalamu wa Rasilimali za maji kote nchini kuhakikisha wanakuwa na maandalizi ya kutosha kuelewa athali zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Maelezo hayo ameyatoa wakati akifungua mafunzo ya uchambuaji wa takwimu za uwingi na ubora wa maji ambayo yanayoendelea jijini Dodoma.

Mhandisi Sanga amesema taifa limepitia katika kipindi cha upungufu wa mvua ambapo kipindi hicho kinapaswa kuwa funzo maalumu la kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mmeona hivi karibuni mwezi wa Novemba, 2021 na Desemba, 2021 tulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo. Haya yote yalisababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, wataalamu mnapaswa kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko hayo,” Mhandisi Sanga amesema.

Amesema sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha tunajenga mabwawa kuwezesha kuvuna maji ya mvua na hivyo kupunguza uhaba wa maji.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Mto Nile, Mhandisi Sylivester Matemu ameshukuru serikali ya Tanzania kwa kuwa makini katika kupangana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Amesema jiografia ya nchi ya Tanzania inatoa nafasi ya kuwa eneo muhimu katika kupambana na kuhakikisha mabadiliko ya tabia nchi hayaathili maendeleo ya bonde la mto Nile.

Amesema sehemu kubwa ya ziwa Victoria iko upande wa Tanzania na chanzo cha mto Nile ni Ziwa Victoria. Hivyo, bonde la mto Nile liendelee kuwa salama lazima watanzania wahakikishe wanalinda vyanzo vya maji vinavyochangia uhai wa mto huo.

Kitengo cha Mawasiliano