Habari

Imewekwa: Apr, 29 2022

Wanasheria wa Sekta ya Maji Watakiwa Kuendana na Mageuzi ya Kisekta

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka Wataalam wa Sheria wa Sekta ya Maji kuzipitia upya sheria za maji na kuziboresha ikibidi ili kuendana na kasi ya mageuzi ya kisekta.

Ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Wanasheria wa Sekta ya Maji mkoani Morogoro.

Waziri Aweso amesema mabadiliko na mageuzi makubwa yanayoendelea kwenye Sekta ya Maji yanahitaji Wanasheria kujituma zaidi na kuongeza ufanisi kwenye majukumu yao, huku akiwataka kuzijua vizuri sheria pamoja na kuzitafsiri kwa mustkabali mzuri wa sekta.

Akisema kuwa zipo changamoto mbalimbali katika Sekta ya Maji ikiwa ni pamoja na upotevu wa maji unaochangiwa na wizi wa maji, uharibifu wa miundombinu ya majisafi na usimamizi mzuri wa mikataba ya miradi mbalimbali na kuzingatia thamani ya fedha.

Akisema kuwa Wanasheria wana mchango muhimu sana katika kufanikisha malengo ya Sekta ya Maji katika kuepusha na kutatua migogoro ya kiutumishi, utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma.

Aidha, Waziri Aweso amesema kwa sasa Sekta ya Maji ina Wanasheria 55 ambao wameajiriwa na wizara na taasisi 23 tu zilizo chini ya wizara na kuzielekeza taasisi zote kuweka na kutekeleza mipango ya kuajiri wanasheria wenye sifa na weledi ili kutekeleza majukumu ya kisheria kwa ufanisi.

Awali, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka amesema malengo ya kikao ni kufahamiana, kubadilishana uzoefu na mbinu za kikazi pamoha na kuongezeana uwezo katika maeneo mbalimbali ya kitaalam na kiutumishi.

Akisema kuwa kikao hicho ni cha pili mara baada ya kikao cha kwanza kilichofanyika Septemba, 2018 ambacho pamoja na masuala mbalimbali kilipitia na kutoa maoni kuhusu mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5/2019 ambayo inatumika sasa.