Habari

Imewekwa: Feb, 11 2026

Tumieni Mifumo ya Kiteknolojia Kudhibiti Upotevu wa Maji – Mhandisi Kundo

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew (Mb), amewataka watendaji wa Sekta ya Maji nchini kutumia mifumo ya kisasa ya kiteknolojia kubaini na kudhibiti upotevu wa maji pamoja na kusimamia viwango na ubora wa vifaa vinavyotumika katika utekelezaji wa miradi ya maji, ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Mhandisi Kundo ametoa maelekezo hayo mkoani Manyara wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Gharama za Uwekezaji wa Huduma za Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (WASH), unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 94.62 katika kipindi cha miaka mitano.

Amesema mpango huo umeainisha hali ya sasa ya huduma, mahitaji yaliyopo, malengo yanayotarajiwa kufikiwa pamoja na rasilimali zitakazohitajika ili kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Hanang wanapata huduma bora ya majisafi, vyoo salama na mazingira yenye afya.

Amesisitiza kuwa katika jitihada za kuboresha huduma na kupunguza malalamiko ya wateja kuhusu ankara za maji, mamlaka za maji na vyombo vya watumia maji vinapaswa kuongeza kasi ya ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla (prepaid meters) pamoja na kuimarisha ufanisi katika utendaji kazi ili kuziba mianya ya upotevu wa maji, ikiwemo mivujo katika miundombinu.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Gridi ya Maji ya Taifa unaolenga kuunganisha na kuimarisha mifumo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa maji nchini, hatua itakayoongeza uhakika na usalama wa upatikanaji wa maji katika maeneo yote nchini.

Mhandisi Kundo ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi, imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kupitia ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji mijini na vijijini.

Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa sekta hiyo kushirikiana kwa karibu na wadau pamoja na wananchi kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo unakuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, amelipongeza Shirika la WaterAid Tanzania kwa kuratibu maandalizi ya mpango huo.