Habari

Imewekwa: Feb, 11 2026

Kamati ya Kudumu ya Bunge Yaridhishwa na Mikakati ya Ulinzi wa Rasilimali za Maji

News Images

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Wizara ya Maji kwa hatua mbalimbali inazochukua, ikiwemo utekelezaji wa ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya Kamati kupokea na kujadili taarifa ya Wizara kuhusu namna inavyotekeleza majukumu yake ya kulinda, kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji nchini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Jackson Kiswaga (Mb), amesema ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji ni hatua muhimu itakayowezesha upatikanaji wa maji ya kutosha katika maeneo mbalimbali ya nchi, pamoja na kusaidia kulinda vyanzo vya maji ambavyo vimekuwa vikiharibiwa na shughuli za kibinadamu. Aidha, ameisisitiza Wizara kuhakikisha inasimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ili kuzuia vitendo vinavyoathiri vyanzo vya maji.

Awali, akiwasilisha taarifa ya Wizara kuhusu utunzaji, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema Wizara imedhamiria kuhakikisha ujenzi wa gridi hiyo unakamilika kwa wakati.

Amesema utekelezaji wa mpango huo unaendelea vizuri na unahusisha sekta zote katika mnyororo wa matumizi ya maji, ikiwemo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na Wizara ya Nishati.

Amesisitiza kuwa mpango huo utawezesha makundi yote katika jamii kufikiwa kwa utaratibu mzuri utakaoepusha migongano ya matumizi ya rasilimali za maji. Aidha, ameomba ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.