Habari

Imewekwa: Feb, 11 2026

Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vya Sekta za Maji na Nishati Kuimarisha Ushirikiano

News Images

Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vya Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati vimekubaliana kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi na kuboresha huduma kwa wananchi.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Maji, Mtumba, jijini Dodoma.

Akiongoza kikao hicho, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maji, Diana Kimario, pamoja na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Nishati, Bi. Anitha Ishengoma, walikubaliana kuendelea kushirikiana katika kufuatilia na kutathmini miradi mbalimbali ya sekta za maji na nishati ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

“Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati tumekuwa tukifanya kazi kwa ukaribu kwa muda mrefu, hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama Bwawa la Mwalimu Nyerere na Bwawa la Kidunda,” amesema Bi. Kimario.

Kwa upande wake, Anitha Ishengoma amesema ni muhimu kwa vitengo hivyo kuhakikisha sera na mipango ya wizara pamoja na taasisi zake zinatekelezwa ipasavyo ili kurahisisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji na nishati kwa wananchi.

Naye Mchumi Mwandamizi kutoka Wizara ya Maji, Bw. Alex Kikarugaa, amesema miradi ya maji imepiga hatua kubwa, ambapo kwa sasa kiwango cha upatikanaji wa maji kimefikia asilimia 92.5 katika maeneo ya mijini na asilimia 85.2 katika maeneo ya vijijini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na watendaji mbalimbali kutoka vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vya wizara zote mbili, kikiwa na lengo la kuendeleza ushirikiano wa kitaasisi ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji na nishati nchini.