Habari

Imewekwa: Aug, 11 2025

Umoja na Ushirikiano Ndio Chachu ya Mafanikio ya Wizara ya Maji – Mkurugenzi Akyoo

News Images

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Maji, Christina Akyoo, amesema mafanikio ya wizara hiyo yanatokana na umoja na ushirikiano wa taasisi zote zilizopo chini yake katika kutekeleza majukumu ya msingi.

Mkurugenzi Akyoo ametoa kauli hiyo lwakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Nanenane, yenye kaulimbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”, yanayoendelea katika Uwanja wa John Samwel Malecela, jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mkurugenzi Akyoo amefafanua kuwa mshikamano na ushirikiano wa taasisi zote za wizara hiyo umekuwa chachu ya maendeleo ya Sekta ya Maji.

“Ndiyo maana Banda la Wizara ya Maji kwenye Maonesho ya Nanenane limejumuisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Chuo cha Maji, Mfuko wa Taifa wa Maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, pamoja na Maabara ya Ubora wa Maji. Mafanikio ya sekta hii yanategemea mshikamano na ushirikiano wa taasisi hizi zote,” Mkurugenzi Akyoo amesema. Akiongeza kuwa uwakilishi wa taasisi zote za Wizara ya Maji katika maonesho hayo unathibitisha umoja na shirikiano wa Sekta hiyo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa Wizara ya Maji katika Maonesho ya Nanenane, akibainisha kuwa sekta hiyo ni mdau muhimu na mtambuka kwa sababu maji ni rasilimali ya msingi kwa maendeleo ya sekta zote, ikiwemo kilimo.

Mkurugenzi Akyoo ameongeza kuwa Wizara ya Maji inashirikiana kwa karibu na sekta nyingine ili kuhakikisha mchango wake unaleta matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa.

Sikukuu ya Nanenane huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Agosti. Maadhimisho ya mwaka huu yamehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho yaliyofanyika jijini Dodoma.