Habari
Visima vya Akiba Vyaunganishwa Kwenye Mfumo wa Maji Ili Kupunguza Changamoto Dar
Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb), amewataka wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki cha upungufu wa maji, akibainisha kuwa hali hiyo ni ya mpito na inashughulikiwa kwa kasi.
Akiwa katika ziara ya kukagua hali ya upatikanaji maji jijini Dar es Salaam, Mhe. Aweso amesema dhamira ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote kwa wakati. Amesisitiza umuhimu wa watumishi wa sekta ya maji kufanya kazi kwa weledi, bidii na ushirikiano ili changamoto zinazojitokeza zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
“Mhe. Rais ametuagiza kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana kusaidia wananchi katika kipindi hiki. Ni vita tunayopigana kuhakikisha kila mtu anapata maji safi na salama. Tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maji yaliyopo yanawafikia wananchi,” Waziri Aweso amesema.
Katika ziara hiyo, Mhe. Aweso ametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Kimara, Magufuli Hosteli (UDSM), Bunju, Kawe na Mwananyamala. Ametoa uhakikisho kuwa baadhi ya maeneo tayari yameanza kupokea maji, na kwamba visima vya akiba vinaendelea kuunganishwa kwenye mfumo wa usambazaji ili kupunguza adha inayowakumba wananchi.
Ameeleza kuwa bado kuna maeneo ambayo huduma haijarejea kikamilifu, lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha kila sehemu inafikiwa na maji.
“Tumeshuhudia matanki yakiwa na maji na tumepata taarifa za huduma kurejea kwenye baadhi ya maeneo. Wananchi wote ambao bado hawajafikiwa, nawahakikishia kuwa huduma itarejea. Tutahakikisha maji yanayopatikana yanahifadhiwa na kusambazwa ipasavyo,” Waziri Aweso amesisitiza.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa maji ni uhai, na Serikali itaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kila kijiji, mtaa na kaya inafikiwa na huduma ya maji kwa usahihi na kwa wakati.

