Habari

Imewekwa: Dec, 08 2025

Mto Ruvu Ubaki Kwa Matumizi ya Binadamu Tu – RC Kunenge

News Images

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ametoa wito kwa wakulima wanaotumia maji ya Mto Ruvu kwa shughuli za kilimo kusitisha matumizi hayo kwa muda, hadi pale mvua zitakapoanza kunyesha kwa wingi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuepusha athari kwa uzalishaji na usambazaji wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Mhe. Kunenge alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika mitambo ya uzalishaji maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu, kwa ajili ya kukagua hali ya uzalishaji na upatikanaji wa maji katika chanzo cha Mto Ruvu.

Amesema mabadiliko ya tabianchi hususan kuongezeka kwa joto, yamesababisha kupungua kwa kiwango cha maji katika maeneo ya Ruvu Chini, hali inayoathiri uzalishaji wa maji. Aidha, shughuli za kilimo zisizo rasmi kando kando ya mto na zisizo na vibali zimechangia kuongeza changamoto hiyo.

“Mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kupungua kwa kiwango cha maji, hasa Ruvu Chini. Hali hii pia inachangiwa na kilimo kisicho rasmi kinachofanyika kando ya mto bila vibali,” RC Kunenge amesema.

Ameongeza kuwa uzalishaji wa maji katika mtambo wa Ruvu Chini umepungua ingawa si kwa kiwango kikubwa huku mtambo wa Ruvu Juu ukiendelea kuwa na kiwango cha maji cha kuridhisha.

“Natoa wito kwa watumiaji wa maji, hasa wanaofanya kilimo, kusitisha matumizi ya maji ya mto kwa muda hadi mvua zitakapoanza. Kwa sasa maji haya yabaki kwa matumizi ya binadamu tu. Pia tutafuatilia wale wanaojihusisha na kilimo bila vibali na kusababisha changamoto katika mto,” Kunenge amesema.

Amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa maji, kwa kuwa bwawa hilo litahifadhi maji ya kutosha bila kutegemea mvua za msimu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amelitaka Bonde la Wami–Ruvu kwa kushirikiana na DAWASA kuchukua hatua za haraka kuboresha maeneo yenye changamoto katika Mto Ruvu yanayosababisha upotevu wa maji na kupungua kwa mtiririko, ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji ya uhakika.