Habari
Tanzania Yaunga Mkono Uendelevu wa Bonde la Mto Nile
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza msimamo wake thabiti wa kuendelea kuiunga mkono Jumuiya ya Bonde la Mto Nile (Nile Basin Initiative – NBI), ikibainisha kuwa rasilimali za maji katika bonde hilo ni msingi muhimu wa uchumi, usalama wa chakula na ustawi wa jamii katika nchi zote wanachama.
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi, Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), amesema Tanzania inaamini katika dhana ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji kama njia ya kuhakikisha usawa wa matumizi na ulinzi wa vyanzo vya maji vinavyotegemewa na mamilioni ya watu.
Amesema kuwa kizazi cha sasa kina wajibu wa kihistoria wa kulinda utoaji endelevu wa maji ya Mto Nile ili kuendeleza uchumi, kilimo, nishati na maisha ya watu katika mataifa yote yanayoufafanua mto huo, akisisitiza kuwa mustakabali wa bonde hilo unategemea ushirikiano wa dhati, mazungumzo ya wazi na maamuzi ya pamoja.
Mhandisi Kundo ameongeza kuwa mipango ya pamoja ya usimamizi wa rasilimali za maji ikiwemo ukusanyaji wa takwimu, ufuatiliaji wa mazingira, usanifu wa miradi ya pamoja na ujenzi wa miundombinu ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha usalama na upatikanaji endelevu wa maji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kila nchi kutimiza wajibu wa kuchangia fedha kwa wakati ili kuiwezesha NBI kutekeleza miradi yake ipasavyo, akibainisha kuwa uwiano wa michango na uwajibikaji wa kifedha ni msingi wa kuimarisha uaminifu na uendelevu wa miradi ya kikanda.
Hata hivyo, Mhandisi Kundo ameeleza kuwa ili Bonde la Nile liendelee kuwa na tija, kunahitajika mshikamano thabiti na utatuzi wa pamoja wa changamoto kama mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko wa ardhi, matumizi yasiyo endelevu ya maji, pamoja na kuhakikisha kuwa matumizi ya rasilimali hii adhimu yanazingatia usawa, haki, uwajibikaji na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

