Habari

Imewekwa: Sep, 23 2025

Mwenge Wazindua Mradi wa Maji Mkigo wa Zaidi ya Sh. Bilioni 1 Kigoma

News Images

Mwenge wa Uhuru umezindua rasmi Mradi wa Maji Mkigo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma. Mradi huo umetekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa ufadhili wa Mfuko wa Taifa wa Maji kwa kushirikiana na Mpango wa Malipo kwa Matokeo (PforR).

Mradi wa Mkigo umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.9 na unatarajiwa kuwanufaisha wananchi wapatao 14,705 katika kijiji cha Mkigo na vijiji jirani. Lengo kuu ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, jambo linaloendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, aliipongeza RUWASA kwa usimamizi na utekelezaji bora wa mradi huo. Alisisitiza kuwa mradi wa Mkigo ni kielelezo cha dhahiri cha jitihada za Serikali kuondoa kero ya maji vijijini na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.

“Miradi ya aina hii inaleta suluhisho la kudumu kwa wananchi na ni matunda ya mshikamano kati ya Serikali na wadau katika kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi,” Ussi amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Mathius Mwenda, amesema RUWASA itaendelea kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango bora vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

“Tuna dhamira ya dhati kuhakikisha kila kijiji Kigoma kinapata huduma ya majisafi na salama. RUWASA itaendelea kusimamia miradi yote kwa ufanisi ili kufikia lengo la Serikali la kufikisha maji vijijini kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025,” Mhandisi Mwenda amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Vijana na Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Suleiman Mvunye, ambaye pia ni mzaliwa wa kijiji cha Kalinzi, ametoa ushuhuda wa maisha ya kabla ya mradi akieleza changamoto walizokuwa wakipitia.

“Tulikuwa tukitembea zaidi ya kilomita tano kufuata maji ya mto, ambayo mara nyingi hayakuwa salama. Wakati mwingine tulipata magonjwa ya tumbo kutokana na maji hayo. Leo hii tunaona mwanga mpya kupitia mradi huu na tunaishukuru Serikali kwa kutuondolea adha hiyo,” Mvunye amesema kwa furaha.

Uzinduzi wa Mradi wa Maji Mkigo ni sehemu ya shughuli za Mwenge wa Uhuru 2025, unaolenga kufuatilia na kuzindua miradi ya maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi katika sekta mbalimbali zikiwemo maji, afya, elimu na miundombinu.