Habari

Imewekwa: Sep, 21 2025

Bodi ya RUWASA Yataka Usimamizi Mzuri Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii

News Images

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Ruth Koya, ameelekeza Mameneja wa RUWASA wa Mikoa na Wilaya kusimamia vizuri Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) ili kuimarisha huduma ya maji vijijini na kuwa na uwezo wa kuhudumia maeneo makubwa zaidi.

Amesema viongozi na watumishi wa RUWASA, hususan wa ngazi ya mikoa na wilaya, wanapaswa kubadili mtazamo kutoka kufikiria zaidi ujenzi wa miradi pekee na badala yake kuweka mkazo katika usimamizi wa CBWSOs, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya majisafi na salama.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maji kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani, hivyo ni jukumu la viongozi wa RUWASA kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kama ilivyokusudiwa”, Mhandisi Koya amebainisha.

Mhandisi Koya ametoa maelekezo hayo katika ziara ya kikazi ya Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA katika Halmashauri ya Msalala katika Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga. Ziara iliyohusisha pia kikao cha kazi na CBWSOs tatu za Ilogi, Fufumo na Bulyanhulu.

Bodi ilipokea na kujadili taarifa za utendaji kazi wa CBWSOs hizo, ikiwemo mafanikio na changamoto mbalimbali, kisha ikatoa ushauri wa hatua za kuchukua ili kuboresha zaidi huduma ya maji katika maeneo yao.

Katika kikao hicho Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA iliambatana na Menejimenti ya RUWASA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Wolta Kirita, ambaye pia ni Katibu wa Bodi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019 iliyoanzisha RUWASA, taasisi hiyo ina jukumu la kuviwezesha, kuvijengea uwezo na kuvisimamia CBWSOs ili viwe na ufanisi katika utoaji wa huduma na kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata majisafi na salama kwa mujibu wa sheria.