Habari
“Wizara ya Maji Kutoka Wizara ya Lawama, Mpaka Wizara ya Mfano” - Rais Samia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Wizara ya Maji kutoka kuwa Wizara ya Lawama na kuwa Wizara ya mfano, kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya katika kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa watanzania wote.
Rais Samia ametoa pongezi hizo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28 kwa miji ya Handeni, Korogwe, Muheza, na Pangani, iliyofanyika katika eneo lilipojengwa tenki la maji la Mkombozi, Mtaa wa Vibaoni, wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema mwaka 2021 nilikuwa nikiwasukuma sana kwa kuwaambia fanyeni hivi, fanyeni vile. Lakini tangu mwaka 2022 Wizara ya Maji inafanya vizuri sana.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa miradi ya maji, huku akiwataka watendaji wa Sekta ya Maji kuendelea kuchapa kazi kwa bidii.
"Kazi yangu mimi ni kutafuta fedha, na kazi yenu ni utekelezaji. Nawapongeza watendaji wote wa Sekta ya Maji, endeleeni kuchapa kazi." amesema Rais Samia.
Awali, akizungumza mbele ya Rais, Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso amesema Wizara ya Maji imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Rais Samia. Amesema miradi mingi ya maji imeweza kutekelezwa kwa wakati kutokana na utayari wa Rais Samia kuruhusu fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mradi wa maji wa Miji 28 kwa mkoa wa Tanga unatekelezwa na Mkandarasi JWIL Infra Ltd na unasimamiwa na Kampuni ya WAPCOS, zote kutoka India. Mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani milioni 81.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa kidakio cha maji (intake) katika Kijiji cha Mswaha, Wilaya ya Korogwe, ujenzi wa chujio la maji (treatment plant) katika Kijiji cha Tabora, Korogwe, ujenzi wa matenki nane ya maji pamoja na ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilomita 188.
Hadi sasa utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 60, ambapo mabomba yenye urefu wa kilomita 140 yameshalazwa, tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni 2 katika Mtaa wa Vibaoni, Wilaya ya Handeni, limekamilika, na tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 300,000 katika Kijiji cha Ubangaa, Wilaya ya Pangani, limekamilika.
Matenki mengine ya maji katika vijiji vya Bongi, Segera, Kwafungo, Kilulu, Madanga, na Boza yako katika hatua tofauti za utekelezaji.
Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025 na utawezesha upatikanaji wa maji kwa zaidi ya wakazi 860,000 wa vijiji 161 vya Wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza, na Pangani.