Habari
Serikali Yasisitiza Ulinzi na Uhifadhi wa Ziwa Victoria
Waziri Mkuu,, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Ziwa Victoria ni rasilimali ya pamoja inayohitaji kulindwa na kuhifadhiwa kupitia ushirikiano wa kikanda kutokana na mchango wake mkubwa katika uchumi, biashara, mazingira, usalama na ustawi wa maisha ya wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza kama mgeni rasmi katika maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria yaliyofanyika katika Viwanja vya Nanenane, Nyamhongolo, jijini Mwanza, Dkt. Nchemba alisema kuwa ziwa hilo si mali ya nchi moja bali ni urithi wa pamoja unaounganisha mataifa na jamii zinazolizunguka.
“Ziwa Victoria si mali ya nchi moja. Ni rasilimali inayotuunganisha kama jumuiya, hivyo tunapaswa kushirikiana katika kulinda mazingira yake, kuimarisha usalama na kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazolitegemea,” alisema.
Alieleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yanapaswa kuwa jukwaa la kuhamasisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji, kuimarisha mshikamano wa kikanda na kuongeza uwajibikaji wa pamoja katika kulinda mazingira ya ziwa hilo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Dkt. Nchemba pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usalama na uokoaji majini pamoja na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kufuatilia shughuli za uvuvi, ubora wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alizitaka taasisi za utafiti kuendelea kufanya tafiti zitakazochangia upatikanaji wa suluhisho la changamoto zinazoathiri mazingira ya Ziwa Victoria, zikiwemo kuongezeka kwa magugu maji na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika Kanda ya Ziwa pamoja na kuimarisha juhudi za kulinda na kuhifadhi Ziwa Victoria, ambalo ni nguzo muhimu ya uchumi, usalama na maendeleo ya wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kufuatia uamuzi wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa maadhimisho hayo yamejumuisha shughuli mbalimbali za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, ikiwemo upandaji miti, maonesho ya wadau wa sekta ya maji na mijadala ya kitaalamu kuhusu usimamizi na uhifadhi endelevu wa Ziwa Victoria.
Maadhimisho hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda Ziwa Victoria, ambalo ni mojawapo ya rasilimali muhimu zaidi za maji barani Afrika.

