Habari

Imewekwa: Jun, 05 2026

Sekta ya Maji Yapata Mafanikio Makubwa Katika Utekelezaji wa Miradi

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Mathew Kundo (Mb), amewapongeza watumishi wa Sekta ya Maji kwa mchango wao mkubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini. Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za watumishi pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta hiyo.

Mhe. Kundo alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la Wizara ya Maji na taasisi zake katika maonesho ya kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, yanayofanyika katika Viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, alitaja utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kidunda wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 330, pamoja na miradi mingine inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha na kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi.

Aidha, Mhandisi Kundo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha utekelezaji wa zaidi ya miradi 1,206 ya maji yenye thamani ya takriban shilingi trilioni nne. Miradi hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama nchini na kufanikisha azma ya kuwafikishia wananchi huduma hiyo kwa kiwango kikubwa zaidi.

Vilevile, aliwataka wataalamu wa Sekta ya Maji kuendelea kubuni na kutafuta vyanzo vipya vya maji, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza, kuendeleza na kuhifadhi vyanzo vya maji vilivyopo ili kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 5, 2026, ambapo Makamu wa Rais, Mhe. Balozi Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.