Habari

Imewekwa: Sep, 15 2023

Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya maji mkoani Mtwara - Rais Samia

News Images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa maji, wa chujio la maji la mradi wa maji wa Mtwara nakuwahakikishia wananchi wa mkoa huo kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya maji ili kila mkazi anufaike na huduma hiyo muhimu.

Amesema hayo akizungumza na wananchi katika wa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mara baada ya kuzindua mradi huo eneo la Mangamba mjini Mtwara.

Amesema chujio alilolizindua litanufaisha asilimia 80 ya wakazi wa mji wa Mtwara na hivyo kusukuma maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mtwara ili kutatua changamoto ya huduma ya maji.

“ Mahitaji ya maji katika mji wa Mtwara ni lita milioni 18 kwa siku ambapo uzalishaji kwa sasa ni lita milioni 14, na kuna upungufu ni lita milioni 4. Aidha, Serikali imetoa bilioni 19 ili kutatua changamoto hiyo" Aweso amesema.

Amewataka wawekezaji mbalimbali katika sekta ya Viwanda kujitokeza mkoani hapo kwani huduma ya maji imeimarishwa kwa kiasi kikubwa.

"Wananchi wa Mtwara niwaeleza kuwa, pamoja na mafanikio tuliyofikia, Mhe. Rais Samia ameridhia na tutakwenda kutekeleza ndoto mliyoiomba kwa muda mrefu ya kutumia maji ya mto Ruvuma." Waziri Aweso amesisitiza.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara ambapo anakagua,nakuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.