Habari

Imewekwa: Dec, 15 2025

Kundo Aagiza Taasisi Zote Za Sekta Ya Maji Njombe Kuboresha Huduma

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amezitaka taasisi zote za sekta ya maji mkoani Njombe kufanya tathmini ya kina na kuwasilisha takwimu sahihi kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo wanayoyahudumia.

Hatua hiyo inalenga kuiwezesha Wizara ya Maji kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa miradi mipya na kuboresha kwa haraka huduma ya maji kwa wananchi.

Mhandisi Kundo ametoa agizo hilo akiwa mkoani Njombe alipokuwa akizungumza na watumishi kutoka taasisi zote za Sekta ya Maji za mkoa huo. Amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuzingatia kikamilifu agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuhusu ufungaji wa dira za malipo ya kabla (pre-paid meters) kwa wateja wa huduma ya maji.

Amesema kila mtumishi anatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika nafasi yake, huku akisisitiza ushirikiano baina ya taasisi za sekta ya maji pamoja na kujifunza kutoka kwa taasisi zilizofanikiwa katika utekelezaji wa miradi yao.

Aidha, Mhandisi Kundo amesisitiza umuhimu wa kujenga na kudumisha uaminifu kwa wananchi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu huduma ya maji, hatua itakayosaidia kuimarisha mahusiano mazuri kati ya watoa huduma na jamii.

Kikao hicho kimeelezwa kuwa chachu ya kuongeza ari na uwajibikaji katika utendaji kazi wa sekta ya maji mkoani Njombe, ambapo mikakati imejikita katika kukamilisha miradi inayoendelea na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Maelekezo hayo yametolewa kwa lengo la kuhakikisha huduma ya maji mkoani Njombe inaboreshwa kwa haraka na kwa ufanisi, kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa maji unaendelea kwa usawa na endelevu.