Habari

Imewekwa: Dec, 15 2025

Serikali Yataka Mradi wa Maji Mafinga Ukamilike kwa Kasi na Ubora

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb), amemtaka mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 Mafinga, Kampuni ya Jandu Plumbers Ltd, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha wananchi wa Mafinga wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati uliopangwa.

Mhandisi Kundo ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ucheleweshaji katika miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Mradi wa Maji Mafinga ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa Serikali wa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika miji 28 nchini, na unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 48. Kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza upatikanaji wa majisafi na salama katika Mji wa Mafinga kutoka asilimia 67 hadi kufikia asilimia 95.

Naibu Waziri Kundo amesema uwekezaji huo mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, unapaswa kuakisiwa kwa vitendo kupitia kasi ya utekelezaji, ubora wa kazi na kukamilika kwa mradi kwa wakati.

Aidha, Mhandisi Kundo amebainisha kuwa changamoto zote zilizokuwa zikiathiri kasi ya utekelezaji wa mradi huo zimeshatatuliwa, hivyo hakuna sababu ya mkandarasi kuchelewesha kazi. Amemtaka mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika na matarajio ya Serikali pamoja na wananchi wa Mafinga.

Kwa upande wake, amesisitiza kuwa Wizara ya Maji itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa na wananchi wananufaika na huduma bora ya majisafi na salama.