Habari
Rais Dkt. Samia Azindua Sera ya Taifa ya Maji 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002, Toleo la Mwaka 2025 na kusisitiza Sera hiyo iwe kichocheo cha maendeleo ya Sekta ya Maji nchini .
Tukio hilo limefanyika sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani na Kilele cha Wiki ya Maji hapa nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Rais Samia akihutubia maelfu ya washiriki ukumbini na kupitia vyombo mbalimbali vya habari amesema maboresho ya Sera ya Taifa ya Maji ni lazima kwa sababu anuwai zikiwemo ongezeko la watu nchini, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya siasa za Dunia. Hivyo, maboresho hayo yataleta tija na utatuzi wa changamoto za upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa Watanzania.
Akisisitiza kuimarisha usalama wa maji kwa kulinda na kutunza rasilimali za maji kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania na sio Wizara ya Maji pekee. Pamoja na kulinda na kutunza miundombinu ya maji kwa uhakika na kupata huduma ya maji endelevu.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia ameagiza kuanzishwa kwa Gridi ya Maji ya Taifa kwa uhakika wa maji nchini, akisema kuwa hatua hiyo itawezesha maeneo yote kufikiwa na huduma ya uhakika ya maji kwa wakati wote.
“Ninaagiza ianzishwe Gridi ya Maji ya Taifa, ili maji yaweze kufika katika maeneo yote nchini na kumaliza changamoto ya uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo. Agizo hilo na lifanyiwe kazi mara moja”, Rais Samia amesisitiza.
Amehitimisha Maadhimisho ya Siku ya Maji na Wiki ya Maji Kitaifa yaliyokuwa na Kaulimbiu ya “Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa ajili ya Uhakika wa Maji” yenye lengo la kuimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji ambavyo ndio msingi wa uwepo wa maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Aidha, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo ya Kitaifa kwa kuleta Mageuzi katika Sekta ya Maji nchini “Gamechanger” na Wizara ya Maji pamoja na Tuzo ya Kinara wa Maji Afrika na Taasisi ya Water Aid Afrika kwa kutambua mchango wake kwenye Sekta ya Maji barani Afrika. Pia, ameteuliwa na Water Aid Afrika kuwa Mlezi wa Masuala ya Maji na Usafi wa Mazingira wa Bara la Afrika.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa Tanzania yameambatana na Kampeni ya Maji na Wanawake ambayo ilihamasisha shughuli za uvunaji wa maji ya mvua ; uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Bwawa la Kidunda; uzinduzi wa Mradi wa Same-Mwanga-Korogwe awamu ya kwanza; Mapitio ya Utendaji wa Sekta ya Maji 2025; Mkutano wa Tathmini ya Utendaji wa Mamlaka za Maji nchini; pamoja na utiaji saini Mkataba wa Mradi wa Maji katika Mji wa Tunduma.
Kazi hizo zote zimelenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji ili kufikia lengo la asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo Desemba 2025 ambapo kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji ni asilimia 83 vijijini na asilimia 91 mijini.