Habari

Imewekwa: Nov, 20 2025

Teknolojia ya Kisasa Itumike Katika Maombi ya Maunganisho ya Maji - Mhandisi Mwajuma

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri ametaka maombi ya maunganisho mapya yafanyike kwa teknolojia ya kisasa ili kupunguza urasimu na kufikisha huduma kwa wateja kwa wakati.

Akizungumza wakati akihitimisha mafunzo ya maboresho Mfumo Mama wa Utoaji Huduma za Maji Kimtandao (MAJIIS) kwa Wataalam wa Sekta ya Maji ambao umelenga kurahisisha upatikanaji wa huduma, upatikanaji wa taarifa, ufuatiliaji na tathmini pamoja na kuchukua maamuzi kwa haraka na sahihi.

Mhandisi Mwajuma amezitaka Mamlaka za Maji kuacha matumizi ya karatasi kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi ya kukaa muda mrefu kabla ya kuunganishiwa huduma, akiamini kuwa Mfumo wa MAJIIS utakuwa suluhisho ya changamoto hiyo.

Amesema kuwa Wizara itafuatilia kwa ukaribu uzingatiaji wa Mkataba wa Huduma kwa Wateja katika maunganisho ya wateja, ikiwemo kuchukua sahihi za mahali mita zimefungwa ili kuboresha usomaji na kupunguza utoaji bili bila usomaji halisi wa mita. Kwa mujibu wa maelekezo hayo, taasisi pia zimetakiwa kuweka na kuingiza malengo ya mwaka kwenye mfumo, na kuzingatia taratibu za matumizi ili kuepusha hoja za ukaguzi.

Katibu Mkuu Mwajuma amezitaka taasisi zote zinazotumia mfumo huo kuhakikisha zinatumia moduli zote mpya bila visingizio na kuhakikisha watendaji ambao hawakuhudhuria mafunzo wanajifunza kupitia taasisi jirani.

Aidha, Mhandisi Mwajuma amesisitiza kuwa baada ya mafunzo haya, taarifa zote muhimu za uzalishaji, usambazaji, maunganisho, upotevu wa maji na makusanyo zinapaswa kupatikana moja kwa moja kupitia Dashibodi ya MAJIIS badala ya kutumwa kwa njia ya simu au mafaili ya Kompyuta.

Mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Morogoro yamehusisha Wataalam wa Sekta ya Maji kutoka Mamlaka za Maji, Bodi za Maji za Mabonde, Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs), EWURA, Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA) na Wizara ya Teknolojia ya Habari.

Mfumo wa MAJIIS ulianza kutumika mwaka 2020 kufuatia ujenzi wake ulioanza 2019, ukiwa na lengo la kuunganisha mifumo yote ya mapato ya Mamlaka za Maji na kusimamia kwa pamoja huduma za maji nchini. Mwaka 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliuzindua rasmi mfumo huo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji yaliyofanyika Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.

Miongoni maboresho mapya ya MAJIIS yanajumuisha kuanzishwa kwa Moduli ya Uzalishaji Maji, Portal mpya ya Maombi ya Maunganisho Mapya ya Huduma za Maji, Utambuzi wa Maji Yanayopotea pamoja na utengenezaji wa Dashibodi ya MAJIIS kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mamlaka za Maji 85, CBWSOs 950 na Bodi za Maji za Mabonde 9.

Kwa hatua hii mpya, Wizara inalenga kuimarisha uwazi, ufuatiliaji na ufanisi katika usimamizi wa huduma za maji nchini, huku ikikiimarisha chombo cha kidijiti kinachochochea uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.