Habari
Waziri Aweso Ahimiza Matokeo kwa Watumishi Sekta ya Maji
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watumishi wa Sekta ya Maji nchini kuthibitisha imani ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utendaji kazi wenye matokeo.
Aweso ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati wa kikao na mapokezi yake pamoja na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Matthew (Mb) mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Maji, Mji wa Serikali Mtumba.
“Tuzingatie hotuba ya Rais Samia kwa Sekta ya Maji kwa kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yetu ili kuhakikisha huduma za majisafi na usafi wa mazingira zinawafikia wananchi wote kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili”, Aweso amesema na kusisitiza kujitoa kuna baraka zaidi.
Amewataka watumishi wote kushikamana, kufanya kazi kwa uadilifu na kasi kwa sababu Sekta ya Maji inagusa uhai wa kila Mtanzania, hivyo utekelezaji wa miradi ya maji ni lazima uende kwa kasi na ubora.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Matthew (Mb) amewataka watumishi kuthibitisha takwimu za maandiko na uhalisia, kuhakikisha mafanikio ya sekta yanapimika na kuonekana. Akisisitiza umuhimu wa kupunguza malalamiko ya wananchi kwa kutoa huduma bora na kuwafikia kwa wakati.
“Mafanikio tunayoyatafuta hayatakuja kwa bahati. Yatatokana na kujituma katika kazi, nidhamu, mipango mizuri na usimamizi makini wa rasilimali,” amesema Mhandisi Kundo na kusisitiza viongozi wapo kwasababu ya nguvu kubwa ya watumishi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amewapongeza Waziri Aweso na Naibu Waziri Kundo kwa kuendelea kuonesha umahiri wa uongozi na kujitoa kwao katika kuboresha Sekta ya Maji.
Aidha, amewahakikishia kuwa Menejimenti na Watumishi wote wa Sekta ya Maji kuungana nao katika utekelezaji wa majukumu, kusimamia Sera na Malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Sekta ya Maji inaendelea kushika nafasi ya juu katika ajenda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, na chini ya uongozi wa Waziri Aweso, matumaini ya wananchi kupata huduma bora za maji yanaendelea kuimarika.

