Habari
Naibu Waziri Mhandisi Mahundi awaagiza DUWASA kufikisha maji zahanati ya Ntyuka
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph kuhakikisha anafikisha huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza kwenye zahanati ya Ntyuka iliyoko kata ya Ntyuka Jijini Dodoma. Agizo hilo amelitoa wakati akizindua mradi wa maji wa Ntyuka-Chimalaa kwa niaba ya Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb). Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya shilingi Milioni 471.8
Amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha inamtua mama ndoo ya maji kichwani huku ikifikisha huduma ya majisafi na salama katika maeneo yote ya huduma za kijamii. Kwa maana hiyo Mkurugenzi ahakikishe Zahanati hiyo iliyoko katika eneo la mradi inafikishiwa huduma ya maji haraka iwekanavyo. Amewahakikishia wananchi wa jiji la Dodoma na Tanzania kwa ujumla kuwa serikali itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha huduma za kijamii zinafikiwa na huduma ya majisafi na salama.
Aidha, amewapongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira Dodoma kwa kusimamia vizuri hadi kukamilika kwa mradi huo.
Awali akitoa taarifa ya mradi Mhandisi Joseph amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza imekamilika na inahudumia wakazi wapatao 1,931 katika maeneo ya Ntyuka mtaa wa Chimalaa. Awamu ya pili inatarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/24 na itanufaisha wakazi wapatao 2,510 wa mtaa wa Nyerere na hivyo kufanya jumla ya wanufaika wa mradi huo kufikia 4,441.