Habari

Imewekwa: Nov, 01 2019

Naibu Waziri Aweso Ataka Mradi wa Maji Jibondo Ukamilike Haraka

News Images

Pwani: 01 Novemba, 2019

TAARIFA KWA UMMA

Mkandarasi wa Kampuni ya Elegance Developers Ltd anayefanya kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Jibondo kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.95 katika Kata ya Jibondo, Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani ametakiwa kukamilisha mradi huo kabla ya mwaka 2019 kuisha kwa kuwa fedha za kumlipa zipo.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametoa maagizo hayo alipokuwa ziarani katika Wilaya ya Mafia na kubaini kuchelewa kukamilika kwa mradi huo, uliotakiwa kukamilika Disemba, 2018 ilhali wananchi wa Kata ya Jibondo wakikabiliwa na tatizo kubwa la maji.

Naibu Waziri Aweso amesema pamoja na changamoto zilizotajwa mradi haukutakiwa kuchukua muda mrefu kiasi hicho, akimuhakikishia mkandarasi kumlipa milioni 276 anazodai kwa sasa, lakini na yeye ahakikishe maji yanatoka baada kulipwa fedha hizo.

‘‘Nimeona uhalisia wa Jibondo kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kunusuru hali wananchi hawa, Serikali haipo tayari kuona wananchi wake wakiteseka wakati fedha za ujenzi wa miradi ya maji si tatizo’’, amesema Aweso.

“Nataka wataalam wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kusimamia kazi hii kwa karibu, nataka kabla mwaka huu 2019 haujaisha maji yawe yanatoka Jibondo na huduma iwe inapatikana kwa asilimia 100’’, amesisitiza Aweso.

Wananchi wa Kata ya Jibondo wamesema wamefarijika kuona Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya maji, lakini wameomba mradi huo ukamilike kwa kuwa umechukua muda mrefu kutokana na changamoto za kutafuta maji zinazotokana hali ya kijiografia ya eneo hilo ambalo ni kisiwa tofauti na maeneo mengine yenye vyanzo vya maji mazuri.

Kitengo cha Mawasiliano