Habari

Imewekwa: Sep, 09 2021

Mradi wa Maji wa Miji 28 Kuanza Hivi Karibuni Asema Aweso

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema serikali imeanza maandalizi ya kutekeleza mradi wa kimkakati kwenye miji 28 hapa nchini ili kuhakikisha huduma ya majisafi inamfikia kila mtanzania.

Amesema hayo leo alipokutana na Wahariri na Waandishi wa Habari wa mkoa wa Dodoma katika kikao kazi ambacho kililenga kuonesha mageuzi makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea katika sekta ya maji, pia kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kuhabarisha umma kuhusu maendeleo yanayofanywa na serikali.

Waziri Aweso amesema serikali imepokea Dola za Marekani milioni 500 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni moja ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka serikali ya India kupitia Benki ya Exim India kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji katika miji 28 na kwamba kibali cha utekelezaji wa mradi huo kimeshatolewa.

“Dhamira ya Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kumtua mama ndoo kichwani. Tunamshukuru sana kwa kuendelea kutupatia fedha nyingi. Hivi karibuni ametuongezea fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 207 mbali na shilingi bilioni 680 iliyoidhinishwa na Bunge la bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022,” Waziri Aweso amesema.

Aidha Waziri Aweso amezungumzia utekelezaji wa miradi ya maji vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambapo alinainisha kwamba kiasi cha shilingi bilioni 450 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mikataba katika miradi 1,176 ili kuongeza hali ya upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 72.3 ya sasa hadi kufikia asilimia 77 ifikapo mwaka 2022.

“Lengo la serikali ni kwamba ifikapo 2025 upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijini ifikie asilimia 85 na mweleko ni mzuri,” Waziri Aweso amesema.

Waziri Aweso amesema wakati RUWASA inaanzishwa mwaka 2019 ilirithi jumla ya miradi 177 kutoka kwenye Halmashauri kote nchini na hadi sasa hivi miradi 115 imeshakamilika na miradi 62 inatarajiwakukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2021.

Kitengo cha Mawasiliano