Habari

Imewekwa: Apr, 28 2026

Wizara ya Maji Yaanza Utekelezaji Kufikisha Maji Vijiji 1,575

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amezindua rasmi mradi mkubwa wa maji wa Badilisha Maisha, Mpwapwa wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 30, ukiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inawafikia wananchi wengi zaidi, hususan katika vijiji ambavyo bado havijapata huduma hiyo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma, Waziri Aweso amesema Serikali imelenga kufikisha huduma ya maji katika vijiji 1,575 vilivyosalia kufikia mwaka 2030, ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa wa uhakika na endelevu nchini kote. 

Amesema mradi wa Badilisha Maisha Mpwapwa ni sehemu ya utekelezaji wa lengo hilo, ambapo utanufaisha zaidi ya wananchi 156,000 katika vijiji 23, pamoja na shule 11 na vituo vya afya 10. Mradi huo unahusisha ujenzi wa mifumo 9 ya maji, vituo 255 vya kuchotea maji na uunganishaji wa huduma ya maji kwa kaya zenye uhitaji maalum. 

Kwa mujibu wa Aweso, utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama, utapunguza magonjwa ya mlipuko, kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi pamoja na kuinua kiwango cha elimu kutokana na wanafunzi kupata muda zaidi wa kushiriki masomoni.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi, viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na taasisi husika kuhakikisha wanalinda na kuitunza miundombinu ya maji ili kudumisha uendelevu wa huduma hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika hatua nyingine, ametoa shukrani kwa Shirika la Water For People Tanzania kwa kushirikiana na Serikali katika kufanikisha mradi huo, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Mradi wa Badilisha Maisha Mpwapwa unaendelea kuwa mfano wa miradi muhimu inayochangia kufikia dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya majisafi na salama.