Habari

Imewekwa: Apr, 27 2026

Mhandisi Mwajuma Waziri Ashinda Tuzo ya Malkia wa Nguvu

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ametunukiwa Tuzo ya Utumishi Bora wa Umma katika kilele cha utoaji wa Tuzo za Malkia wa Nguvu kwa Kanda ya Kati, zilizofanyika jijini Dodoma.

Tuzo hiyo imetolewa na Kampuni ya Habari na Burudani ya Clouds (Clouds Media Group) Aprili 26, 2026, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa wanawake walioonesha utendaji uliotukuka katika sekta mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo zilizowakutanisha wadau wa maendeleo, viongozi wa serikali na wanawake wajasiriamali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Dkt.Nchimbi amewapongeza washindi wote na kuishukuru Clouds Media Group kwa kuendelea kuibua na kutambua juhudi za wanawake nchini.

Aidha, amewataka Watanzania kuachana na dhana potofu ya kumchukulia mwanamke kama kiumbe dhaifu, badala yake watambue mchango mkubwa wa wanawake katika kukuza uchumi wa Taifa.

Akimtaja Mhandisi Mwajuma Waziri kama mfano, amesema ni kielelezo cha mwanamke shupavu aliyebadilisha utendaji kazi na kuleta matokeo chanya katika Sekta ya Maji nchini.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushika nafasi za uongozi na kufanya vizuri katika utumishi wa umma.

Tuzo za Malkia wa Nguvu kwa mwaka huu zimejikita katika kuwatambua wanawake walioleta mabadiliko makubwa katika jamii kupitia nyanja za uongozi, biashara na huduma za kijamii.