Habari

Imewekwa: Apr, 27 2026

ZAMCOM Wakutana Tanzania

News Images

Maji ya kimataifa yanazidi kuthibitisha kuwa ni moja ya rasilimali muhimu zinazoleta umoja, ushirikiano na maendeleo kati ya nchi mbalimbali na wananchi wao.

Waziri wa Maji wa Tanzania, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), akifungua kikao cha 13 cha Baraza la Mawaziri la Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (ZAMCOM) jijini Dar es Salaam, amesisitiza kuwa maji hayana mipaka na yana uwezo mkubwa wa kukusanya watu na nchi kwa ajili ya maendeleo ya pamoja.

Mhe. Aweso, ambaye pia ni Mwenyekiti wa mkutano huo, alisema kuwa umoja na ushirikiano kati ya wananchi na nchi zinazogawana maji ya kimataifa umeletwa na maji yanayovuka mipaka ya nchi zao. Aliongeza kuwa maji ya bonde la mto Zambezi yamekuwa ni kiungo muhimu cha kuunganisha nchi wanachama na kuwaletea maendeleo yanayoonekana.

“Ni muhimu sana kuwa na rasilimali za maji za kutosha na kuzitumia kwa busara ili kuleta maendeleo katika nchi zetu. Wananchi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika kutunza na kuhifadhi rasilimali hii ili iweze kuendeleza sekta nyingine za uchumi kama kilimo, nishati, uvuvi, utalii na biashara,” alisema Waziri Aweso.

Alisisitiza kwa wajumbe wa mkutano huo kuwa maji si tu hitaji la kimsingi la maisha, bali ni chombo chenye nguvu cha kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wote.

ZAMCOM ni kamisheni inayosimamia usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji katika bonde la mto Zambezi. Inagusa moja kwa moja maisha ya zaidi ya milioni 51 ya watu katika nchi wanachama zifuatazo: Tanzania, Angola, Zambia, Malawi, Namibia, Botswana, Zimbabwe na Msumbiji (Mozambique).

Mkutano huu wa 13 unatarajiwa kujadili masuala muhimu yanayohusu usimamizi wa maji, changamoto za mabadiliko ya tabianchi, miradi ya maendeleo ya pamoja, na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama ili kuhakikisha bonde la Zambezi linatoa faida sawa na endelevu kwa kila nchi na raia wake.