Habari

Imewekwa: Aug, 07 2020

Mamlaka za Maji Nchini Zatakiwa Kuiga Mfano Mbeya

News Images

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameridhishwa na ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na wataalam wa ndani (force account) kwenye mkoa wa Mbeya na kuzitaka mamlaka zote za maji kote nchini kuiga mfano huo.

Ameyasema hayo wilayani Rungwe alipohitimisha ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa kwa ushirikiano wa wataalam kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA), Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mbeya na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Rukwa.

“Ninahitaji kuona taasisi zote zikishirikiana kwa pamoja kutimiza lengo la kuwafikishia huduma ya maji kwa wananchi, kama ilivyo hapa Mbeya ambapo tumeona mafanikiomakubwa kwenye miradi mingi yaliyotokana na ushirikiano uliopo baina ya taasisi uliochangia kwa kiasi kikubwa kukwamua miradi iliyokuwa imekwama kwa kipindi cha muda mrefu akiitaja baadhi ya miradi hiyo ya maji kuwa ni Bulongwe, Busokelo, Vwawa-Mlowo, Chitete, Shongo-Mbalizi, Ndalambo, Chunya na Kingili-Kapapa ikiwa ni baada ya wakandarasi waliokuwa wakiitekeleza kushindwa kuikamilisha kwa wakati na hivyo kusitishiwa mikataba”, ameeleza Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alifurahishwa na maendeleo ya kazi za ujenzi wa miradi mkoani Mbeya na kutoa wito kwa mamlaka nyingine nchini zijifunze uzoefu wa utekelezaji wa miradi ya maji Mbeya, ambayo mingi imeanza kutoa huduma ama imebaki asilimia chache kukamilika tangu mfumo wa force account uanze kutumika.

Akisema kuwa mfumo wa force account una faida kuu tatu; kutumia gharama nafuu, muda mfupi wa utekelezaji na kutoa matokeo makubwa ambayo ndiyo maana halisi ya kutumia force account tofauti na wakandarasi wababaishaji, huku akitoa wito kwa wataalam wote wa ndani wanaosimamia ujenzi wa miradi kwa mfumo huo kuzingatia viwango vya ubora na ujenzi wa miradi endelevu itakayodumu na kutoa huduma kwa miaka mingi.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe,Chalya Nyangindu ameeleza kuwa kiasi cha Sh. bilioni 17 zimetolewa na Serikali kwa wilaya hiyo kwa ajili wa utekelezaji wa miradi ya maji na kuishukuru kwa kuwa zimeleta mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Maji katika wilaya hiyo na kumuomba Katibu Mkuu Sanga kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingi zaidi.