Habari

Imewekwa: Nov, 08 2023

​Maafisa Maendeleo ya Jamii ni Msingi katika Utekelezaji wa Miradi ya Maji - Aweso

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka Mameneja wa mikoa na wilaya wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwawezesha na kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii katika hatua zote za utekelezaji wa miradi ya maji kwa kuwa wao ndio kiungo muhimu na jamii

Ametoa maelekezo hayo leo tarehe 08 Novemba , 2023 akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii katika eneo la utoaji huduma endelevu ya maji na usafi wa mazingira vijijini katika ukumbi wa Jiji, Mtumba mkoani Dodoma.

Pia, amewataka Watendaji wote kuanzia ngazi ya wizara,mikoa na wilaya kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini ili wawe sehemu ya malengo ya wizara ya katika kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa majisafi Vijijini ifikapo mwaka 2025 na waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mhe. Aweso akizungumzia mafanikio ya miradi ya maji ya Matokeo kwa malipo (P4R) amewapongeza watendaji wa RUWASA kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo, ambapo Tanzania imekuwa kinara wa Dunia usimamizi na utekelezaji katika nchi zote zinazotekeleza Mpangowa P4R Duniani.

Kitengo cha Mawasiliano