Habari
Katibu Mkuu Asaini Makubaliano ya Utendaji na Bodi za Maji za Mabonde

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesaini makubaliano ya utendaji baina ya Wizara ya Maji na Bodi za Maji za Mabonde kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Akizungumza katika halfa fupi ya utiaji saini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa St. Gaspar jijini Dodoma Mhandisi Sanga amesema lengo la kusaini makubaliano ya utendaji ni kuweka viashiria vya kupima utekelezaji wa malengo ambayo Bodi za Maji za Mabonde zimejiwekea na kuwezesha Wizara kufanya tathmini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Bodi za Maji za Mabonde.
Amesema sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji imezipatia Bodi za Maji za Mabonde jukumu la usimamizi wa rasilimali za maji nchini.
“Hakikisheni mnasimamia rasilimali za maji pamoja na vyanzo, endapo usimamizi wa rasilimali za maji hautafanyika kwa makini na kwa uhakika, hakutakuwa na maji ya kugawa na kusambaza na hakutakuwa na maendeleo thabiti na endelevu”, Mhandisi Sanga amesema.
Ameongeza kuwa Bodi za Maji za Mabonde ni mtekelezaji na msimamizi wa moja kwa moja katika kuhakikisha rasilimali za maji zilizopo zinaendelea kuwepo kwa ajili ya matumizi ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, Mhandisi Sanga amewaagiza Maafisa Maji wa Bodi za Maji za Mabonde kusimamia kikamilifu rasilimali za maji, kudhibiti uchafuzi na kuhakikisha matumizi sahihi ya maji kwa ajili ya maendeleo.
Pamoja na hayo, Mhandisi Sanga amesisitiza Bodi hizo kufanya tathmini za uhakika wa rasilimali za maji nchini, kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, kudhibiti uchafuzi katika vyanzo vya maji, kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kusimamia matumizi sahihi na yenye ufanisi ya maji, kushiriki na kulinda maslahi, udugu na ujirani mwema katika usimamizi wa rasilimali za maji shirikishi.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini