Habari
Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira kung'amua endapo maji ya Mtera yanatosha kuhudumia Jiji la Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira imetembelea Bwawa la Mtera kwa lengo la kujiridhisha iwapo maji hayo yanatosha kuanzisha mradi wa maji ambao utasaidia kuongeza uzalishaji wa maji kwa ajili ya kuhudumia Jiji la Dodoma.
Ziara hiyo imefanyika leo Mei 6, 2023 ikihusisha wataalamu kutoka Wizara ya Maji na Sekta mtambuka ikiwemo Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya bwawa hilo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) amesema kamati hiyo imeangalia na kupitia taarifa mbalimbali za watalamu, na watakaa tena pamoja wajadiliane ili maamuzi yatakayofanyika yasiathiri shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
Amesema wanatambua umuhimu wa bwawa hilo katika kuzalisha nishati ya umeme na pia wanatambua mahitaji makubwa ya maji katika jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi lakini wanawajibu wa kuhakikisha uamuzi utakaofanyika hauathiri eneo lolote.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amepongeza kamati hiyo kwa kuamua kutembelea eneo hilo ili kuwa na wazo la pamoja ambalo litasaidia kuondoa adha ya huduma ya maji kwa wananchi.
Amesema Wizara ya Maji inaendelea na hatua mbalimbali ikiwemo kupata ushauri wa Mtaalamu mshauri ili maamuzi yatakayo fanyika yasiathirii shughuli nyingine za kijamii.
Amesema mahitaji ya jiji la Dodoma ni lita za ujazo milioni 133 kwa siku ambapo kwa sasa jiji linazalisha lita za ujazo milioni 68 kwa siku.
Kiwango kitakachochukuliwa katika mradi huo ni lita za ujazo milioni 130 kwa siku. Amesema bado Wizara ya Maji inaendelea na mipango mbalimbali kuhakikisha jiji la Dodoma linaondokana na changamoto ya huduma ya maji.